Kutoka kwa Omari bin Khattwabi Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- Hadithi Marfu'u: "Hakika matendo yote huzingatiwa nia, na hakika kila mtu hulipwa kwa lile alilolinuia, atakayekuwa kuhama kwake ni kwaajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi (malipo yake yatakuwa) ni kwaajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na atakayekuwa kuhama kwake ni kwaajili ya dunia au ataipata au kwaajili ya mwanamke ili amuoe, basi kuhama kwake kutakuwa ni kwa lile alilolihamia".
Kutoka kwa bin Shammasa Al Mihriy Amesema:Tulifika kwa Amru bin Aaswi naye akiwa katika safari ya kifo, akalia kwa muda mrefu, na akageuza uso wake kuelekea ukutani, mwanaye akaanza kusema, Ewe baba yangu, kwani hakukubashiria Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake kwa jambo kadhaa (yaani pepo)? kwani hakukubashiria Mtume-Rehema na Amani ziwe juu yake kwa jambo kadhaa? akageuka kwa uso wake, kisha akasema: Hakika jambo bora katika yale tunayoyaandaa ni kushuhudia kuwa Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Hakika mimi nilikuwa katika hali za aina tatu: Nilijikuta mimi kuwa hakuna anayemchukia kwa Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- kuliko mimi, Na hakuna kitu nilichotamani zaidi kama kumtia mikononi ili nimuue, basi lau ningekufa katika hali hiyo ningekuwa ni katika watu wa motoni, Basi Mwenyezi Mungu alipouweka Uislamu moyoni mwangu, nilimuendea Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na Amani ziwe juu yake- Kisha nikasema: Nyoosha mkono wako wa kulia ili nikupe utiifu wangu kwako, basi akanyoosha mkono wake wa kulia nikakunja mkono wangu, akasema: "Umekuwaje wewe Amru?" Nikasema: Nilitaka niweke sharti kwanza, akasema: "Unaweka sharti la kitu gani?" Nikasema: Nisamehewe, akasema: "Hivi hukujua kuwa uislamu hufuta makosa yaliyokuwa kabla yake, na kuwa kuhama kunafuta makosa yaliyokuwa kabla yake, nakuwa Hija hufuta makosa yaliyokuwa kabla yake?" Kuanzia hapo hapakuwa tena na yeyote niliyempenda zaidi kuliko Mtume wa Mwenyezi Mungu -Rehema na Amani ziwe juu yake- wala niliyemuheshimu zaidi machoni mwangu kuliko yeye, Na sikuwa naweza kumtazama kwa macho yangu; kwasababu ya kumuheshimu, na hata kama ningeombwa nimsifie nisingeweza; kwasababu mimi sikuwa naweza kumtazama kwa macho yangu, na lau ningekufa katika hali hiyo ningetaraji kuwa miongoni mwa watu wa peponi, Kisha tukatawala mambo ambayo mpaka sasa sijui hali yangu ndani yake? Basi ikiwa nitakufa nisifuatwe na maombolezo wala moto, na mkinizika, basi nimwagieni udongo kidogo kidogo, kisha bakini kaburini kwangu kwa kiasi cha muda wa kuweza kumchinja ngamia na kumchuna, na kugawanywa nyama yake, ili nijiliwaze kwenu, na nisubiri nini nitawajibu wajumbe wa Mola wangu.
Kutoka kwa Abuu Huraira radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- Hadithi Marfu'u-: "Namuapa yule ambaye nafsi ya Muhammadi iko mkononi mwake, hatonisikia yeyote katika umma huu, Myahudi wala Mkristo, kisha akafa haliyakuwa hajayaamini yale niliyotumwa kwayo, ispokuwa atakuwa ni katika watu wa motoni".
Kutoka kwa Abuu Huraira radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, Hadithi Marfu'u: "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anapata wivu, na wivu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni kuyafanya mtu yale aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu kwake yeye"
Kutoka kwa Anasi na Abuu Huraira -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao- Hadithi Marfu'u: "Hawezi kuamini mmoja wenu mpaka niwe napendeka kwake zaidi kuliko mtoto wake, na mzazi wake, na watu wote".
Kutoka kwa Jariri bin Abdillahi -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- Amesema: Nilimpa utiifu Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- juu ya kusimamisha swala, na kutoa zaka, na kumnasihi kila muislamu.
Kutoka kwa Abuu Dhari -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- Amesema: Nilikuwa pamoja na Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- katika ardhi yenye mawe katika mji wa Madina, tukaelekea mlima Uhudi, akasema: "Ewe Abuu Dhari" nikasema: Labbaika (nimekuitikia) Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Akasema: "Hainifurahishi mimi kumiliki dhahabu mfano wa mlima huu wa Uhudi, zikapita siku tatu nikawa hata na dinari moja (katika mali hiyo) isipokuwa kiasi ninachokihifadhi kwaajili ya kulipa deni, isipokuwa niseme kwa waja wa Mwenyezi Mungu hivi na vile." akigeuka kuliani kwake na kushotoni kwake, na nyuma yake, kisha akatembea, Akasema: "Hakika wenye vingi ndio wenye vichache siku ya kiyama isipokuwa atakayezungumza kwa mali hivi na vile hivi na vile" akageuka kuliani kwake na kushotoni kwake na nyuma yake, "Na wachache katika wao" kisha akasema kuniambia "Bakia hapo usitoke mpaka nikujie" kisha akaondoka katika giza la usiku mpaka akapotelea, nikasikia sauti imenyanyuka, nikapata hofu isijekuwa kuna mtu kamvamia Mtume -Rehema na Amani ziwe juu yake- nikataka kumfuata nikakumbuka kauli yake "Bakia hapo usitoke mpaka nikujie" nikabakia mpaka aliponijia, nikasema: Nilisikia sauti nikaingiwa na hofu sana, nikamuelezea akasema: "Hivi uliisikia?" Nikasema: Ndiyo, akasema: "Huyo ni Jibril alinijia akasema: Atakayekufa katika umma wako hamshirikishi Mwenyezi Mungu na kitu chochote ataingia peponi" Nikasema: Hata akizini na akaiba? Akasema: "Hata akizini na akaiba".
Kutoka kwa Anas -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-: Yakwamba Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake- na Mua'dh akiwa nyuma yake juu ya kipandwa, Alisema: "Ewe Mua'dh" Akasema: Labaika Wasa'daika- Nimekuitikia kwa furaha yako- Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Alisema: "Ewe Mua'dh" Akasema: Labaika Wasa'daika- Nimekuitikia kwa furaha yako- Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Alisema: "Ewe Mua'dh" Akasema: Labaika Wasa'daika- Nimekuitikia kwa furaha yako- Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Alisema hivyo mara tatu, Akasema: "Hakuna mja yeyote atakayeshuhudia kuwa Hapana Mola ispokuwa Mwenyezi Mungu, nakuwa Muhammadi ni mja wake na ni Mtume wake kiukweli toka moyoni mwake ispokuwa atamharamisha Mwenyezi Mungu kuingia motoni" Akasema: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu hivi nisiwaeleze watu hili ili wajipe bishara (matumaini)? Akasema: "Basi watabweteka" Akalizungumza hilo Mua'dh wakati wa kifo chake kwa kuhofia kupata dhambi.
Kutoka kwa Omari bin Khattwab na mwanaye Abdillahi na Abuu Huraira -Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao- Hadithi Marfu'u: "Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka washuhudie kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu nakuwa Muhammadi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na wasimamishe swala, na watoe zaka, pindi watakapofanya hivyo watakuwa wamezikinga kutokana nami damu zao na mali zao isipokuwa kwa haki ya uislamu na hesabu yao itakuwa juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu".
Kutoka kwa Abuu Dhari Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- Kutoka kwa Mtume Rehema na Amani ziwe juu yake- katika yale anayoyapokea kutoka kwa Mola wake: "Enyi waja wangu hakika Mimi nimeharamisha dhulma juu ya Nafsi yangu na nikaifanya kuwa ni haramu baina yenu, basi msidhulumiane, enyi waja wangu nyote ni wapotevu isipokuwa yule niliye muongoza, basi niombeni uongofu nami nitakuongozeni, enyi waja wangu nyote ni wenye njaa isipokuwa yule niliye mlisha, basi niombeni chakula nami nitakulisheni, enyi waja wangu nyote mpo uchi isipokuwa yule niliye mvisha, basi niombeni kuvishwa nami nitakuvisheni, enyi waja wangu hakika nyinyi mnakosea usiku na mchana na mimi ninasamehe madhambi yote, basi niombeni msamaha nami nitakusameheni, enyi waja wangu hamtafikia kufanya madhara mpaka mnidhuru wala hamtafanya mambo yenye manufaa mpaka mninufaishe, enyi waja wangu laiti wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu binadamu na majini wakijikusanya wote wakawa na ucha Mungu wa mtu mmoja hilo lisinge niongezea chochote katika Ufalme wangu, enyi waja wangu laiti wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu binadamu na majini wakijikusanya wote wakafanya uovu wa mtu mmoja hilo lisinge punguza chochote katika Ufalme wangu, enyi waja wangu laiti wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu binadamu na majini wangejikusanya katika uwanja mmoja wakaniomba nikampa kila mtu alicho kiomba hilo lisinge punguza chochote katika Ufalme wangu isipokuwa ni kama sindano inavyo punguza maji pindi inapo ingizwa baharini, enyi waja wangu si vinginevyo bali hakika matendo yenu yote nina wahifadhieni kisha nitawapa malipo yenu, mwenye kupata kheri amshukuru Mwenyezi Mungu, na atakayepata kinyume na hayo basi asimlamu yeyote isipokuwa nafsi yake) ((360)).